2 Wafalme 22
1 Yosia alikuwa na umri wa miaka minane alipoanza kutawala; akatawala miaka thelathini na mmoja katika Yerusalemu; na jina la mama yake aliitwa Yedida, binti Adaya wa Bozkathi.
2 Akafanya yaliyo mema machoni pa Bwana, akaenda katika njia yote ya Daudi baba yake, wala hakugeuka upande wa kuume wala wa kushoto.
3 Ikawa, katika mwaka wa kumi na nane wa mfalme Yosia, mfalme akamtuma Shafani, mwana wa Azalia, mwana wa Meshulamu, mwandishi, nyumbani kwa Bwana, akisema,
4 Enenda kwa Hilkia, kuhani mkuu, ili aihesabu fedha yote inayoletwa nyumbani mwa Bwana, ambayo mabawabu wameipokea kwa watu;
5 tena waitie ile fedha katika mikono ya wafanya kazi wanaoisimamia nyumba ya Bwana; wakapewe wafanya kazi waliomo ndani ya nyumba ya Bwana, ili wapate kupatengeneza mahali palipobomoka ndani ya nyumba;
6 wapewe maseremala, na wajenzi, na waashi; ili kununua miti na mawe yaliyochongwa wapate kuitengeneza nyumba.
7 Lakini hawakuulizwa habari za ile fedha waliyokabidhiwa; maana walitenda kazi kwa uaminifu.
8 Naye Hilkia, kuhani mkuu, akamwambia Shafani, mwandishi, Nimekiona kitabu cha torati katika nyumba ya Bwana. Hilkia akampa Shafani kile kitabu, naye akakisoma.
9 Shafani mwandishi akamwendea mfalme, akamletea mfalme habari tena, akasema, Watumishi wako wamezitoa zile fedha zilizoonekana ndani ya nyumba, nao wamewakabidhi wafanya kazi wanaoisimamia nyumba ya Bwana.
10 Kisha Shafani mwandishi akamwambia mfalme, akasema, Hilkia kuhani amenipa kitabu. Shafani akakisoma mbele ya mfalme.
11 Ikawa, mfalme alipokwisha kuyasikia maneno ya kitabu hicho cha torati, alirarua nguo zake.
12 Mfalme akamwamuru Hilkia kuhani, na Ahikamu, mwana wa Shafani, na Akbori, mwana wa Mikaya, na Shafani mwandishi, na Asaya, mtumishi wa mfalme akasema,
13 Enendeni, mkamwulize Bwana kwa ajili yangu, na kwa ajili ya watu hawa, na kwa ajili ya Yuda yote, katika habari za maneno ya kitabu hiki kilichoonekana; kwa kuwa hasira ya Bwana ni kubwa aliyotukasirikia, kwa sababu baba zetu hawakuyaangalia maneno ya kitabu hiki, kufanya kama hayo yote tuliyoandikiwa.
14 Basi Hilkia kuhani, na Ahikamu, na Akbori, na Shafani, na Asaya, wakamwendea Hulda, nabii mke, mkewe Shalumu, mwana wa Tikva, mwana wa Harhasi, mtunza mavazi ya mfalme; (naye alikaa Yerusalemu katika mtaa wa pili;) wakasema naye.
15 Akawaambia, Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi; Mwambieni mtu yule aliyewatuma ninyi kwangu,
16 Bwana asema hivi, Tazama, mimi nitaleta uovu juu ya mahali hapa, na juu yao wakaao hapa, naam, maneno yote ya kitabu alichokisoma mfalme wa Yuda;
17 kwa sababu wameniacha mimi, wameifukizia uvumba miungu mingine, ili wapate kunikasirisha kwa kazi yote ya mikono yao; kwa hiyo hasira yangu itawaka juu ya mahali hapa, isizimike.
18 Lakini yule mfalme wa Yuda, aliyewatuma ninyi kumwuliza Bwana, mtamwambia hivi, Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Kwa habari ya maneno yale uliyoyasikia,
19 kwa kuwa moyo wako ulikuwa mwororo, nawe ukajinyenyekesha mbele za Bwana, hapo ulipoyasikia maneno niliyoyanena juu ya mahali hapa, na juu ya wenyeji wake, ya kwamba watakuwa ukiwa na laana, nawe ulizirarua nguo zako, ukalia mbele zangu; basi, mimi nami nimekusikia wewe, asema Bwana.
20 Kwa hiyo tazama, nitakukusanya pamoja na baba zako, nawe utawekwa kaburini mwako kwa amani; wala macho yako hayatauona uovu huo wote nitakaouleta juu ya mahali hapa. Basi wakamletea mfalme habari tena.