2 Wafalme 17
1 Katika mwaka wa kumi na mbili wa Ahazi mfalme wa Yuda Hoshea mwana wa Ela alianza kutawala juu ya Israeli katika Samaria; akatawala miaka kenda.
2 Akafanya yaliyo maovu machoni pa Bwana, ila si kama wafalme wa Israeli waliomtangulia.
3 Naye Shalmanesa mfalme wa Ashuru akakwea juu yake, Hoshea akawa mtumishi wake, akampa kodi.
4 Mfalme wa Ashuru akaona fitina katika huyo Hoshea; kwa maana alikuwa ametuma wajumbe kwa So, mfalme wa Misri, wala hakumletea kodi mfalme wa Ashuru, kama alivyofanya mwaka kwa mwaka; kwa hiyo mfalme wa Ashuru akamfunga, akamtia kifungoni.
5 Ndipo mfalme wa Ashuru akakwea katikati ya nchi yote, akaenda Samaria, akauhusuru miaka mitatu.
6 Katika mwaka wa kenda wa Hoshea, huyo mfalme wa Ashuru akautwaa Samaria, akawahamisha Israeli mpaka Ashuru, akawaweka katika Hala na Habori, karibu na mto wa Gozani, na katika miji ya Wamedi.
7 Yalitukia hayo kwa sababu wana wa Israeli walikuwa wametenda dhambi juu ya Bwana, Mungu wao, aliyewaleta kutoka katika nchi ya Misri watoke chini ya mkono wa Farao mfalme wa Misri, wakawaacha miungu mingine.
8 Wakaziendea sheria za mataifa, ambao Bwana aliwafukuza mbele ya wana wa Israeli, na sheria za wafalme wa Israeli walizozifanya.
9 Tena, wana wa Israeli wakafanya kwa siri mambo yasiyokuwa mema juu ya Bwana, Mungu wao, wakajijengea mahali pa juu katika miji yao yote, kutoka mnara wa walinzi hata katika miji yenye boma.
10 Wakajisimamishia nguzo na maashera juu ya kila mlima mrefu, na chini ya kila mti wenye majani mabichi;
11 wakafukiza uvumba huko katika kila mahali pa juu, kama mataifa walivyofanya, ambao Bwana aliwafukuza mbele yao; wakaunda mambo mabaya, ili wamkasirishe Bwana;
12 wakatumikia sanamu, ambazo Bwana aliwakataza, akasema, Msitende jambo hili.
13 Pamoja na hayo Bwana aliwashuhudia Israeli, na Yuda, kwa kinywa cha kila nabii, na cha kila mwonaji, akisema, Geukeni, na kuziacha njia zenu mbaya, mkazishike amri zangu na hukumu zangu, sawasawa na ile sheria yote niliyowaamuru baba zenu, nikawapelekea kwa kinywa cha manabii watumishi wangu.
14 Walakini hawakutaka kusikia, bali walifanya shingo zao kuwa ngumu, kama shingo za baba zao, wasiomwamini Bwana, Mungu wao.
15 Wakazikataa sheria zake, na agano lake, alilolifanya na baba zao; na shuhuda zake alizowashuhudia; wakafuata ubatili, wakawa ubatili, nao wakaandamana na mataifa waliowazunguka, ambao Bwana alikuwa amewaagiza, wasitende kwa mfano wao.
16 Wakaziacha amri zote za Bwana, Mungu wao, wakajifanyizia sanamu za kusubu, yaani, ndama mbili, wakafanya na Ashera, wakaliabudu jeshi lote la mbinguni, wakamtumikia Baali.
17 Wakawapitisha watoto wao, waume na wake, motoni, wakapiga ramli, wakafanya uchawi, wakajiuza nafsi zao wapate kufanya yaliyo maovu machoni pa Bwana, hata kumkasirisha.
18 Kwa hiyo Bwana akawaghadhibikia Israeli sana, akawahamisha mbali na uso wake; wala hapana aliyesalia ila kabila ya Yuda peke yake.
19 Hata na watu wa Yuda hawakuyashika maagizo ya Bwana, Mungu wao, lakini walikwenda katika amri za Israeli walizokuwa wamezifanya wenyewe.
20 Basi Bwana akakikataa kizazi chote cha Israeli, akawatesa, na kuwatia katika mikono ya watu wenye kuwateka nyara, hata alipokwisha kuwatupa, watoke machoni pake.
21 Maana aliwatenga mbali Israeli na nyumba ya Daudi; nao wakamfanya Yeroboamu mwana wa Nebati kuwa mfalme; Yeroboamu akawavuta Israeli wasimfuate Bwana, akawakosesha kosa kubwa.
22 Nao wana wa Israeli wakaendelea katika dhambi zote za Yeroboamu alizozifanya; hawakujiepusha nazo;
23 hata Bwana akawaondoa Waisraeli wasiwe mbele zake, kama vile alivyosema kwa kinywa cha watumishi wake wote, manabii. Basi Waisraeli walichukuliwa mateka kutoka nchi yao wenyewe, waende nchi ya Ashuru, hata leo.
24 Naye mfalme wa Ashuru akaleta watu kutoka Babeli, na Kutha, na Ava, na Hamathi, na Sefarvaimu, akawaweka katika miji ya Samaria badala ya wana wa Israeli; wakaumiliki Samaria, wakakaa katika miji yake.
25 Basi ikawa, wakati ule walipoanza kukaa huko, hawakumcha Bwana; kwa hiyo Bwana akapeleka simba kati yao, nao wakawaua baadhi yao.
26 Kwa hiyo wakamwambia mfalme wa Ashuru, wakasema, Wale wa mataifa uliowahamisha, na kuwaweka katika miji ya Samaria, hawaijui kawaida ya Mungu wa nchi; kwa hiyo amepeleka simba kati yao, na tazama, wanawaua, kwa sababu hawaijui kawaida ya Mungu wa nchi.
27 Ndipo mfalme wa Ashuru akatoa amri, akasema, Mpelekeni mmojawapo wa makuhani, mliowachukua kutoka huko; aende akakae huko, akawafundishe kawaida ya Mungu wa nchi.
28 Basi mmoja wa makuhani waliochukuliwa kutoka Samaria akaenda akakaa katika Betheli, akawafundisha jinsi ilivyowapasa kumcha Bwana.
29 Lakini pamoja na hayo watu wa kila taifa wakajifanyia miungu yao wenyewe, wakaiweka katika nyumba za mahali pa juu, walipopafanya Wasamaria, kila taifa katika miji yao walimokaa.
30 Watu wa Babeli wakafanya Sukoth-benothi kuwa mungu wao, watu wa Kutha wakafanya Nergali, watu wa Hamathi wakafanya Ashima,
31 Waavi wakafanya Nibhazi na Tartaki; nao Wasefarvi wakawaunguza wana wao katika moto kwa Adrameleki na Anameleki, miungu ya Sefarvaimu.
32 Basi hivyo wakamcha Bwana, nao wakijifanyia wengine wao kuwa makuhani wa mahali pa juu, ambao waliwafanyia dhabihu katika nyumba za mahali pa juu.
33 Wakamcha Bwana, na kuitumikia miungu yao wenyewe, sawasawa na kawaida za mataifa ambao wao walihamishwa kutoka kwao.
34 Hata siku hii ya leo hufanya sawasawa na kawaida za kwanza; wala hawamwogopi Bwana, wala hawazifuati sheria zao, wala hukumu zao, wala ile torati, wala ile amri Bwana aliyowaamuru wana wa Yakobo, ambaye alimpa jina la Israeli;
35 hao ambao Bwana alifanya agano nao, akawaamuru, akasema, Msiche miungu mingine, wala kuisujudia, wala kuitumikia, wala kuitolea sadaka;
36 ila yeye Bwana, aliyewaleta kutoka nchi ya Misri kwa nguvu nyingi, na kwa mkono ulionyoshwa, yeye ndiye mtakayemcha, yeye ndiye mtakayemsujudia, yeye ndiye mtakayemtolea sadaka;
37 na sheria, na hukumu, na torati, na amri, alizowaandikia, hizo ndizo mtakazozishika na kuzifanya hata milele; wala msiche miungu mingine.
38 Na hilo agano nililofanya nanyi, msilisahau; wala msiche miungu mingine;
39 lakini Bwana, Mungu wenu, ndiye mtakayemcha; naye atawaokoa mikononi mwa adui zenu wote.
40 Walakini hawakusikia, bali wakafanya sawasawa na kawaida zao za kwanza.
41 Basi mataifa hawa wakamcha Bwana, tena wakaziabudu sanamu zao za kuchongwa; na wana wao vile vile, na wana wa wana wao; kama walivyofanya baba zao, wao nao hufanya vivyo hivyo hata leo.