«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »

2 Mambo ya Nyakati 32

1  Ikawa, baada ya mambo hayo, na uaminifu huo, Senakeribu, mfalme wa Ashuru, akaja, akaingia katika Yuda, akafanya marago juu ya miji yenye maboma, akadhania kwamba ataipata iwe yake.

2  Basi Hezekia, alipoona ya kuwa Senakeribu amekuja, na kuazimia kupigana na Yerusalemu,

3  akafanya shauri na wakuu wake, na mashujaa wake, kuzuia maji ya chemchemi zilizokuwa nje ya mji; nao wakamsaidia.

4  Wakakusanyika watu wengi, wakazizuia chemchemi zote, na kijito kilichopita kati ya nchi, wakisema, Kwa nini, wakifika wafalme wa Ashuru, waone maji mengi?

5  Akapiga moyo konde, akaujenga ukuta wote uliobomoka, akauinua sawa na minara, na ukuta wa pili nje, akaongeza nguvu ya Milo, katika mji wa Daudi, akafanya silaha na ngao tele.

6  Akaweka maakida wa vita juu ya watu, akawakusanya kwake uwandani penye lango la mji, akawafurahisha mioyo; akisema,

7  Iweni hodari, na wa moyo mkuu, msiogope, wala msifadhaike kwa sababu ya mfalme wa Ashuru, wala kwa majeshi yote walio pamoja naye; kwa maana yupo mkuu pamoja nasi kuliko aliye pamoja naye;

8  kwake upo mkono wa mwili; ila kwetu yupo Bwana, Mungu wetu, kutusaidia, na kutupigania mapigano yetu. Na watu wakayategemea maneno ya Hezekia, mfalme wa Yuda.

9  Na baada ya hayo Senakeribu mfalme wa Ashuru, akatuma watumishi wake waende Yerusalemu, (naye alikuwapo mbele ya Lakishi, na uwezo wake wote pamoja naye,) kwa Hezekia, mfalme wa Yuda, na kwa Yuda wote waliokuwako Yerusalemu, kusema,

10  Senakeribu, mfalme wa Ashuru, asema hivi, Mwatumainia nini hata mkae mkihusuriwa katika Yerusalemu?

11  Siye Hezekia anayewashawishi, mtolewe kufa kwa njaa na kwa kiu, akisema, Bwana, Mungu wetu, atatuokoa na mkono wa mfalme wa Ashuru?

12  Si yeye Hezekia huyo aliyeondoa mahali pake pa juu, na madhabahu zake, akawaamuru Yuda na Yerusalemu, akisema, Abuduni mbele ya madhabahu moja, na juu yake mtafukiza uvumba?

13  Je! Ninyi hamjui mimi na baba zangu tuliyowafanyia watu wote wa nchi? Je! Miungu ya mataifa wa nchi iliweza kuokoa kwa lo lote nchi zao na mkono wangu?

14  Ni yupi miongoni mwa miungu ya mataifa wale walioharibiwa kabisa na baba zangu, aliyeweza kuwaokoa watu wake na mkono wangu, hata Mungu wenu aweze kuwaokoa ninyi na mkono wangu?

15  Basi sasa asiwadanganye Hezekia, wala asiwashawishi kwa hayo, wala msimwamini; kwa kuwa hapana mungu wa taifa lo lote, wala wa ufalme wo wote, aliyeweza kuwaokoa watu wake na mkono wangu, au na mkono wa baba zangu; sembuse Mungu wenu atawaokoaje ninyi na mkono wangu?

16  Na watumishi wake wakazidi kusema juu ya Bwana Mungu, na juu ya Hezekia, mtumishi wake.

17  Tena akaandika waraka, kumtukana Bwana, Mungu wa Israeli, na kumwambia, akisema, Kama vile miungu ya mataifa wa nchi isivyowaokoa watu wao na mkono wangu, vivyo hivyo Mungu wa Hezekia hatawaokoa watu wake na mkono wangu.

18  Wakawalilia kwa sauti kuu, kwa lugha ya Kiyahudi, watu wa Yerusalemu waliokuwako ukutani ili kuwaogofisha, na kuwafadhaisha; hata wapate kuutwaa mji.

19  Wakamnenea Mungu wa Yerusalemu, kana kwamba kuitaja miungu ya mataifa wa nchi, iliyo kazi ya mikono ya watu.

20  Na kwa ajili ya hayo Hezekia mfalme, na Isaya nabii, mwana wa Amozi, wakaomba, wakalia hata mbinguni.

21  Naye Bwana akatuma malaika aliyewakatia mbali mashujaa wote, na majemadari, na maakida, matuoni mwa mfalme wa Ashuru. Basi akarudia nchi yake mwenye haya ya uso. Naye alipoingia nyumbani mwa mungu wake, wale waliotoka viunoni mwake mwenyewe wakamwangamiza humo kwa upanga.

22  Ndivyo Bwana alivyomwokoa Hezekia, na wenyeji wa Yerusalemu, na mkono wa Senakeribu, mfalme wa Ashuru, na mikononi mwa wote, akawaongoza pande zote.

23  Watu wengi walimletea Bwana zawadi huko Yerusalemu, na vitu vya thamani kwa Hezekia, mfalme wa Yuda; hata yeye akatukuka tangu wakati ule machoni pa mataifa yote.

24  Katika siku hizo Hezekia akaugua akawa katika hatari ya kufa; akamwomba Bwana; naye akasema naye, akampa ishara.

25  Walakini kadiri alivyofadhiliwa Hezekia hakumrudishia vivyo; kwa kuwa moyo wake ulitukuka; kwa hiyo ikawako hasira juu yake, na juu ya Yuda na Yerusalemu.

26  Hata hivyo Hezekia akajinyenyekeza kwa ajili ya huku kutukuka kwa moyo wake, yeye na wenyeji wa Yerusalemu, hata haikuwajia hasira ya Bwana siku za Hezekia.

27  Naye Hezekia akawa na mali nyingi mno na heshima; akajifanyizia hazina za fedha, na za dhahabu, na za vito, na za manukato, na za ngao, na za namna zote za vyombo vya thamani;

28  ghala pia za mazao ya nafaka na mvinyo na mafuta; na malisho ya wanyama wa namna zote, na makundi mazizini.

29  Tena akajifanyizia miji, na mali za kondoo na ng'ombe kwa wingi; maana Mungu alimtajirisha sana sana.

30  Naye huyo Hezekia ndiye aliyezuia chemchemi ya juu ya maji ya Gihoni, akayaleta chini moja kwa moja upande wa magharibi wa mji wa Daudi. Akafanikiwa Hezekia katika kazi zake zote.

31  Walakini kwa habari ya wajumbe wa wakuu wa Babeli, waliotuma kwake kuuliza ajabu iliyofanywa katika nchi, Mungu akamwacha, ili amjaribu, ili kwamba ayajue yote yaliyokuwamo moyoni mwake.

32  Basi mambo yote ya Hezekia yaliyosalia, na matendo yake mema, tazama, yameandikwa katika maono ya Isaya nabii, mwana wa Amozi, katika kitabu cha wafalme wa Yuda na Israeli.

33  Hezekia akalala na babaze, wakamzika mahali pa kupandia makaburi ya wana wa Daudi; nao Yuda wote na wenyeji wa Yerusalemu wakamfanyia heshima alipokufa. Na Manase mwanawe akatawala mahali pake.

«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »
“Neema ya Bwana Yesu na iwe pamoja nanyi.” — 1 Wakorintho 16:23