2 Mambo ya Nyakati 31
1 Basi hayo yote yalipokwisha, wakatoka Israeli wote waliokuwako waende miji ya Yuda, wakazivunja-vunja nguzo, wakayakata-kata maashera, wakabomoa mahali pa juu na madhabahu katika Yuda yote na Benyamini, katika Efraimu pia na Manase, hata walipokwisha kuviharibu vyote. Ndipo wana wa Israeli wote wakarudi, kila mtu kwa milki yake, mijini kwao.
2 Hezekia akaziweka zamu za makuhani na Walawi kwa zamu zao, kila mtu kwa kadiri ya huduma yake, makuhani na Walawi pia, kwa sadaka za kuteketezwa na kwa sadaka za amani, kutumika, na kushukuru, na kusifu, malangoni mwa matuo ya Bwana.
3 Tena akaweka sehemu ya mfalme ya mali zake kwa sadaka za kuteketezwa, yaani, sadaka za kuteketezwa za asubuhi na jioni, na sadaka za kuteketezwa za sabato, na za mwezi mpya, na sikukuu, kama ilivyoandikwa katika torati ya Bwana.
4 Tena akawaamuru watu waliokaa Yerusalemu, watoe sehemu ya makuhani na Walawi, ili hao wajibidiishe katika torati ya Bwana.
5 Mara ilipotangaa amri, wana wa Israeli wakatoa kwa wingi malimbuko ya nafaka, na divai, na mafuta, na asali, na mazao yote ya mashamba; na zaka za vitu vyote wakazileta nyingi.
6 Nao wana wa Israeli na Yuda, waliokaa mijini mwa Yuda, wakaleta pia zaka za ng'ombe na kondoo, na zaka za vitu vilivyowekwa wakfu, alivyowekewa Bwana, Mungu wao, wakaviweka chungu chungu.
7 Katika mwezi wa tatu wakaanza kuweka misingi ya hizo chungu, wakazimaliza katika mwezi wa saba.
8 Hata walipokuja Hezekia na wakuu, na kuziona zile chungu, wakamhimidi Bwana, na watu wake Israeli.
9 Ndipo Hezekia akaulizana na makuhani na Walawi katika habari ya hizo chungu.
10 Azaria kuhani mkuu, wa nyumba ya Sadoki, akamjibu, akasema, Tangu watu walipoanza kuleta matoleo nyumbani kwa Bwana, tumekula na kushiba, na kusaza tele; kwa kuwa Bwana amewabariki watu wake; na kilichosalia ndiyo akiba hii kubwa.
11 Ndipo Hezekia akaamuru kutengeneza vyumba nyumbani mwa Bwana; wakavitengeneza.
12 Wakayaingiza matoleo na zaka na vitu vilivyowekwa wakfu, kwa uaminifu; na juu yake Konania Mlawi alikuwa mkuu, na wa pili ni Shimei nduguye.
13 Na Yehieli, na Azaria, na Nahathi, na Asaheli, na Yerimothi, na Yozabadi, na Elieli, na Ismakia, na Mahathi, na Benaya, walikuwa wasimamizi chini ya mkono wa Konania na Shimei nduguye, kwa amri ya Hezekia mfalme, na Azaria mkuu wa nyumba ya Mungu.
14 Na Kore, mwana wa Imna, Mlawi, bawabu wa mlango wa mashariki, alizisimamia sadaka za hiari za Mungu; ili kugawa matoleo ya Bwana, navyo vitu vilivyokuwa vitakatifu sana.
15 Na chini yake walikuwa Edeni, na Minyamini, na Yeshua, na Shemaya, na Amaria, na Shekania, mijini mwa makuhani, kwa walivyoaminiwa, ili kuwagawia ndugu zao kwa zamu, wakuu na wadogo sawasawa;
16 zaidi ya wale waliohesabiwa kwa nasaba ya wanaume, wenye miaka mitatu na zaidi, kila mmoja aliyeingia nyumbani mwa Bwana, kama ilivyopasa kazi ya kila siku, kwa huduma zao katika malinzi yao, kwa kadiri ya zamu zao;
17 na wale waliohesabiwa kwa nasaba ya makuhani kufuata nyumba za baba zao, na Walawi, wenye umri wa miaka ishirini na zaidi, katika malinzi yao, kwa kadiri ya zamu zao;
18 na wale waliohesabiwa kwa nasaba ya wadogo wao wote, wake zao, na wana wao, na binti zao, katika kusanyiko lote; kwani kwa vile walivyoaminiwa, wakajitakasa katika utakatifu;
19 tena kwa ajili ya wana wa Haruni makuhani, waliokuwamo mashambani mwa malisho ya miji yao, mji kwa mji, kulikuwa na watu waliotajwa majina yao, ili kuwagawia sehemu wanaume wote miongoni mwa makuhani, na wote waliohesabiwa kwa nasaba miongoni mwa Walawi.
20 Na hivyo ndivyo alivyofanya Hezekia katika Yuda yote; akatenda yaliyo mema, na ya adili, na uaminifu, mbele za Bwana, Mungu wake.
21 Na katika kila kazi aliyoanza kwa utumishi wa nyumba ya Mungu, na kwa torati, na kwa amri, ili kumtafuta Mungu wake, aliifanya kwa moyo wake wote, akafanikiwa.