2 Mambo ya Nyakati 27
1 Yothamu alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala; akatawala katika Yerusalemu miaka kumi na sita; na jina la mamaye aliitwa Yerusha binti Sadoki.
2 Akafanya yaliyo ya adili machoni pa Bwana, sawasawa na yote aliyoyafanya Uzia babaye; isipokuwa hakuingia hekaluni mwa Bwana. Lakini watu walikuwa wakali kufanya maovu.
3 Ndiye aliyelijenga lango la juu la nyumba ya Bwana, na juu ya ukuta wa Ofeli akajenga sana.
4 Tena akajenga miji katika milima ya Yuda, na mwituni akajenga ngome na minara.
5 Kisha akapigana na mfalme wa wana wa Amoni, akawashinda. Na wana wa Amoni wakampa mwaka ule ule talanta mia za fedha, na kori elfu kumi za ngano, na elfu kumi za shayiri. Hayo ndiyo waliyomtolea wana wa Amoni, mwaka wa pili pia, na mwaka wa tatu.
6 Basi Yothamu akawa na nguvu, kwa kuwa alizitengeneza njia zake mbele za Bwana, Mungu wake.
7 Na mambo yote ya Yothamu yaliyosalia, na vita vyake vyote, na njia zake, tazama, yameandikwa katika kitabu cha wafalme wa Israeli na Yuda.
8 Alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala; akatawala miaka kumi na sita huko Yerusalemu.
9 Yothamu akalala na babaze, wakamzika katika mji wa Daudi; na Ahazi mwanawe akatawala mahali pake.