2 Mambo ya Nyakati 17
1 Na Yehoshafati mwanawe akatawala mahali pake, akajitia nguvu juu ya Israeli.
2 Akaweka jeshi katika miji yote yenye maboma ya Yuda, akatia na askari walinzi katika nchi ya Yuda, na katika miji ya Efraimu, aliyoitwaa Asa babaye.
3 Naye Bwana alikuwa pamoja na Yehoshafati, kwa kuwa alikwenda katika njia za kwanza za Daudi babaye, asiyatafute mabaali;
4 lakini alimtafuta Mungu wa baba yake, akaenda katika amri zake, wala si katika matendo ya Israeli.
5 Kwa hiyo Bwana akauthibitisha ufalme mkononi mwake; Yehoshafati akaletewa zawadi na Yuda wote; basi akawa na mali na heshima tele.
6 Ukainuliwa moyo wake katika njia za Bwana; na zaidi ya hayo akapaondoa mahali pa juu, na maashera, katika Yuda.
7 Tena, katika mwaka wa tatu wa kutawala kwake, akawatuma wakuu wake, yaani, Ben-haili, na Obadia, na Zekaria, na Nethaneli, na Mikaya, ili kufundisha mijini mwa Yuda;
8 na pamoja nao Walawi, yaani, Shemaya, na Nethania, na Zebadia, na Asaheli, na Shemiramothi, na Yehonathani, na Adonia, na Tobia, na Tob-adonia, Walawi; na pamoja nao Elishama na Yehoramu, makuhani.
9 Wakafundisha katika Yuda, wenye kitabu cha torati ya Bwana; wakazunguka katika miji yote ya Yuda, wakafundisha kati ya watu.
10 Hofu ya Bwana ikaziangukia falme za nchi zote zilizozunguka Yuda, wasipigane vita na Yehoshafati.
11 Na baadhi ya Wafilisti walimletea Yehoshafati zawadi, na fedha ya kodi; Waarabu nao wakamletea makundi, kondoo waume saba elfu na mia saba, na mabeberu saba elfu na mia saba.
12 Ukuu wake Yehoshafati ukazidi sana; akajenga katika Yuda ngome na miji ya hazina.
13 Naye alikuwa na kazi nyingi katika miji ya Yuda; na watu wa vita, watu mashujaa humo Yerusalemu.
14 Na hivi ndivyo walivyohesabiwa kwa mbari za baba zao; wa Yuda, maakida wa maelfu; Adna jemadari, na pamoja naye watu mashujaa mia tatu elfu;
15 na wa pili wake Yehohanani akida, na pamoja naye mia mbili na themanini elfu;
16 na baada yake Amasia mwana wa Zikri, aliyejitoa kwa Bwana kwa moyo, na pamoja naye mia mbili elfu, watu mashujaa;
17 na wa Benyamini; Eliada mtu shujaa, na pamoja naye mia mbili elfu wenye nyuta na ngao;
18 na wa pili wake Yehozabadi, na pamoja naye mia na themanini elfu waliojiweka tayari kwa vita.
19 Hao ndio waliomngojea mfalme, zaidi ya hao mfalme aliowaweka katika miji yenye maboma katika Yuda yote.