1 Samweli 7
1 Na hao watu wa Kiriath-yearimu wakaja, wakalichukua sanduku la Bwana, wakalileta ndani ya nyumba ya Abinadabu huko kilimani, nao wakamtenga Eleazari, mwanawe, ili alilinde sanduku la Bwana.
2 Ikawa, tangu siku hiyo ambayo sanduku lilikaa Kiriath-yearimu wakati ulikuwa mwingi; kwa maana ulikuwa miaka ishirini; na nyumba yote ya Israeli wakamwombolezea Bwana.
3 Basi Samweli akawaambia nyumba yote ya Israeli, akasema, Ikiwa mnamrudia Bwana kwa mioyo yenu yote, basi, iondoleeni mbali miungu migeni, nayo Maashtorethi yatoke kwenu, mkamtengenezee Bwana mioyo yenu, mkamtumikie yeye peke yake; naye atawaokoa katika mikono ya Wafilisti.
4 Ndipo wana wa Israeli wakayaondoa Mabaali na Maashtorethi, wakamtumikia Bwana peke yake.
5 Samweli akasema, Wakusanyeni Israeli wote Mispa, nami nitawaombea ninyi kwa Bwana.
6 Wakakusanyika huko Mispa, wakateka maji na kuyamimina mbele za Bwana; wakafunga siku ile, wakasema huko, Tumemfanyia Bwana dhambi. Samweli akawaamua wana wa Israeli huko Mispa.
7 Hata Wafilisti waliposikia ya kuwa wana wa Israeli wamekusanyika huko Mispa, mashehe wa Wafilisti walipanda juu ili kupigana na Israeli. Nao wana wa Israeli waliposikia, wakawaogopa Wafilisti.
8 Wana wa Israeli wakamwambia Samweli, Usiache kumlilia Bwana, Mungu wetu, kwa ajili yetu, kwamba atuokoe na mikono ya Wafilisti.
9 Ndipo Samweli akatwaa mwana-kondoo mchanga, akamtolea Bwana sadaka ya kuteketezwa nzima; Samweli akamlilia Bwana kwa ajili ya Israeli; Bwana akamwitikia.
10 Hata Samweli alipokuwa akiitoa hiyo sadaka ya kuteketezwa, Wafilisti wakakaribia ili kupigana na Israeli; walakini Bwana akapiga ngurumo, mshindo mkubwa sana, juu ya Wafilisti siku ile, akawafadhaisha; nao wakaangamizwa mbele ya Israeli.
11 Nao watu wa Israeli wakatoka Mispa, wakawafuatia Wafilisti, wakawapiga, hata walipofika chini ya Beth-kari.
12 Ndipo Samweli akatwaa jiwe, na kulisimamisha kati ya Mispa na Sheni, akaliita jina lake Eben-ezeri, akisema, Hata sasa Bwana ametusaidia.
13 Hivyo Wafilisti walishindwa, wasiingie tena ndani ya mipaka ya Israeli; na mkono wa Bwana ulikuwa juu ya Wafilisti siku zote za Samweli.
14 Nayo miji ile Wafilisti waliyokuwa wamewapokonya Waisraeli ilirudishwa tena kwa Israeli, tokea Ekroni mpaka Gathi; na Waisraeli wakauokoa mpaka wake mikononi mwa Wafilisti. Tena kulikuwa na amani kati ya Israeli na Waamori.
15 Naye huyo Samweli akawaamua Israeli siku zote za maisha yake.
16 Naye huenda mwaka kwa mwaka kuzunguka mpaka Betheli, na Gilgali, na Mispa; akawaamua Israeli mahali hapo pote.
17 Na kurudi kwake kulikuwa mpaka Rama; maana ndipo ilipokuwa nyumba yake; nako ndiko alikowaamua Israeli; na huko akamjengea Bwana madhabahu.