1 Samweli 30
1 Ikawa, Daudi na watu wake walipokuwa wamefika Siklagi siku ya tatu, hao Waamaleki walikuwa wameshambulia Negebu, na Siklagi, nao wameupiga Siklagi, na kuuchoma moto;
2 nao wamewachukua mateka wanawake waliokuwamo wakubwa kwa wadogo; hawakuwaua wo wote, ila wakawachukua, wakaenda zao.
3 Basi Daudi na watu wake walipoufikilia mji, tazama, ulikuwa umechomwa moto; na wake zao, na watoto wao, waume kwa wake, wamechukuliwa mateka.
4 Ndipo Daudi na watu waliokuwa pamoja naye wakainua sauti zao na kulia, hata walipokuwa hawana nguvu za kulia tena.
5 Na hao wake wawili wa Daudi walikuwa wamechukuliwa mateka, Ahinoamu wa Yezreeli, na Abigaili, aliyekuwa mkewe Nabali, wa Karmeli.
6 Naye Daudi akafadhaika sana; kwa sababu watu walikuwa wakisema kwamba apigwe kwa mawe, kwa maana nafsi za hao watu wote walisononeka, kila mtu kwa ajili ya wanawe na binti zake; lakini Daudi alijitia nguvu katika Bwana, Mungu wake.
7 Kisha Daudi akamwambia Abiathari, kuhani, mwana wa Ahimeleki, Tafadhali niletee hapa hiyo naivera. Naye Abiathari akamletea Daudi naivera huko.
8 Daudi akauliza kwa Bwana, akasema, Je! Nikiwafuata jeshi hili, nitawapata? Naye akamjibu, Fuata; kwa kuwa hakika utawapata, nawe hukosi utawapokonya wote.
9 Basi Daudi akaenda, yeye na wale watu mia sita waliokuwa pamoja naye, nao wakakifikilia kijito Besori, ambapo wale walioachwa nyuma walikaa.
10 Lakini Daudi akakaza kufuata, yeye na watu mia nne; kwa maana watu mia mbili walikaa nyuma, ambao walitaka kuzimia hata hawakuweza kukivuka hicho kijito Besori.
11 Nao wakamkuta Mmisri mavueni, wakamleta kwa Daudi, na kumpa chakula, naye akala; nao wakampa maji ya kunywa;
12 kisha wakampa kipande cha mkate wa tini, na vishada viwili vya zabibu; naye akiisha kula roho yake ikamrudia; kwa maana alikuwa hakula chakula wala kunywa maji, siku tatu mchana na usiku.
13 Ndipo Daudi akamwuliza, Wewe u mtu wa nani; nawe umetoka wapi? Naye akasema, Mimi ni kijana wa Misri, mtumwa wa Mwamaleki mmoja; bwana wangu aliniacha, kwa sababu tangu siku hizi tatu nalishikwa na ugonjwa.
14 Sisi tulishambulia Negebu ya Wakerethi, na ya milki ya Yuda, na Negebu ya Kalebu; na huo mji wa Siklagi tukauchoma moto.
15 Daudi akamwambia, Je! Wewe utaniongoza chini hata nilifikilie jeshi hilo? Naye akasema, Uniapie kwa Mungu, ya kwamba hutaniua, wala kunitia mikononi mwa huyo bwana wangu, nami nitakuongoza chini hata kulifikilia jeshi hilo.
16 Na hapo alipokuwa amewaongoza chini, tazama, hao walikuwa wametawanyika juu ya nchi yote, wakila na kunywa, na kufanya karamu, kwa sababu ya hizo nyara kubwa walizochukua katika nchi ya Wafilisti, na katika nchi ya Yuda.
17 Naye Daudi akawapiga tangu ukungu wa jioni hata jioni ya siku ya pili; hakuna aliyeokoka, ila vijana mia nne waliopanda ngamia na kukimbia.
18 Daudi akawapokonya wote waliokuwa wamechukuliwa na Waamaleki; naye Daudi akawaokoa wakeze wawili.
19 Wala hawakupotewa na kitu, mdogo wala mkubwa, wana wala binti, nyara wala cho chote walichojitwalia hao; Daudi akavirudisha vyote.
20 Naye Daudi akatwaa makundi yote ya kondoo na ng'ombe, ambao waliwatanguliza mbele ya wanyama wale wengine, wakasema, Hao ndio nyara za Daudi.
21 Kisha Daudi aliwafikilia wale watu mia mbili, waliokuwa wametaka kuzimia, hata wasiweze kumfuata Daudi, wale waliowaacha wakae karibu na kijito cha Besori; nao wakatoka nje ili kumlaki Daudi, na kuwalaki hao watu waliokuwa pamoja naye, naye Daudi alipowakaribia hao watu, aliwasalimu.
22 Ndipo watu waovu wote na wale wasiofaa, miongoni mwa hao waliokwenda pamoja na Daudi, wakasema, Kwa kuwa watu hawa hawakuenda pamoja na sisi, hatutawapa kitu cho chote katika hizo nyara tulizozitwaa tena, isipokuwa kila mtu atapewa mkewe na watoto wake, wawachukue na kwenda zao.
23 Ndipo Daudi akasema, La, ndugu zangu, msitende hivyo katika hizo nyara alizotupa Bwana, ambaye ndiye aliyetuhifadhi, akalitia mikononi mwetu lile jeshi lililokuja kinyume chetu.
24 Tena ni nani atakayewasikiliza ninyi katika jambo hili? Kwa kuwa kama lilivyo fungu lake yeye ashukaye vitani, ndivyo litakavyokuwa na fungu lake huyo akaaye karibu na vyombo; watagawiwa sawasawa.
25 Basi ikawa hivyo tangu siku ile na baadaye; akaiweka iwe amri na agizo la Israeli hata leo.
26 Basi Daudi alipofika Siklagi, aliwapelekea wazee wa Yuda, rafiki zake, sehemu ya nyara, akasema, Angalieni, zawadi yenu katika nyara za adui za Bwana;
27 yaani, kwa hao wa Betheli, na kwa hao wa Ramoth-Negebu, na kwa hao wa Yatiri;
28 na kwa hao wa Aroeri, na kwa hao wa Sifmothi, na kwa hao wa Eshtemoa;
29 na kwa hao wa Rakali, na kwa hao wa miji ya Wayerameeli, na kwa hao wa miji ya Wakeni;
30 na kwa hao wa Horma, na kwa hao wa Korashani, na kwa hao wa Athaki;
31 na kwa hao wa Hebroni, na kwa hao wa kila mahali alipozoelea Daudi mwenyewe na watu wake.