1 Wafalme 13
1 Na tazama, akatoka mtu wa Mungu katika Yuda kwa neno la Bwana, akafika Betheli. Naye Yeroboamu alikuwa akisimama penye madhabahu, afukize uvumba.
2 Basi mtu huyo akapiga kelele juu ya madhabahu, kwa neno la Bwana akasema, Ee madhabahu, madhabahu, Bwana asema hivi, Angalia, mtoto atazaliwa katika nyumba ya Daudi, jina lake Yosia; na juu yako atawachinja makuhani wa mahali pa juu, wanaofukiza uvumba juu yako, na mifupa ya watu itateketezwa juu yako.
3 Akatoa ishara siku ile ile, akasema, Hii ndiyo ishara aliyoinena Bwana, Tazama, madhabahu itapasuka, na majivu yaliyo juu yake yatamwagika.
4 Ikawa, mfalme Yeroboamu alipoyasikia maneno ya yule mtu wa Mungu, alipopiga kelele juu ya madhabahu huko Betheli, alinyosha mkono wake pale madhabahuni, akasema, Mkamateni. Basi ule mkono wake aliounyosha ukakatika, wala hakuweza kuurudisha kwake tena.
5 Madhabahu ikapasuka, majivu ya madhabahuni yakamwagika, sawasawa na ishara aliyoitoa mtu wa Mungu kwa neno la Bwana.
6 Mfalme akajibu, akamwambia yule mtu wa Mungu, Umsihi sasa Bwana, Mungu wako, ukaniombee, ili nirudishiwe mkono wangu tena. Yule mtu wa Mungu akamwomba Bwana mkono wa mfalme ukarudishwa tena, ukawa kama ulivyokuwa kwanza.
7 Mfalme akamwambia mtu wa Mungu, Karibu nyumbani kwangu ujiburudishe, nami nitakupa thawabu.
8 Mtu wa Mungu akamwambia mfalme, Ujaponipa nusu ya nyumba yako, sitaingia pamoja nawe, wala sitakula chakula, wala sitakunywa maji mahali hapa;
9 maana ndivyo nilivyoagizwa kwa neno la Bwana, kusema, Usile chakula cho chote wala usinywe maji, wala usirudi kwa njia ile uliyoijia.
10 Basi akaenda zake kwa njia nyingine, wala hakurudi kwa njia ile aliyoijia Betheli.
11 Basi nabii mmoja mzee alikuwa akikaa katika Betheli; na wanawe wakamwendea wakamwambia kila neno alilolitenda yule mtu wa Mungu siku ile katika Betheli; na maneno aliyomwambia mfalme, hayo nayo walimwambia baba yao.
12 Baba yao akawaambia, Amekwenda zake kwa njia ipi? Kwa maana wanawe walikuwa wameiona njia ile aliyoiendea yule mtu wa Mungu aliyetoka katika Yuda.
13 Akawaambia wanawe, Nitandikieni punda. Wakamtandikia punda, naye akampanda.
14 Akamfuata mtu wa Mungu, akamkuta ameketi chini ya mwaloni, akamwambia, Je! Wewe ndiwe yule mtu wa Mungu aliyetoka katika Yuda? Akamwambia, Mimi ndiye.
15 Akamwambia, Karibu kwangu nyumbani, ule chakula.
16 Naye akamwambia, Siwezi kurudi pamoja nawe, wala kuingia pamoja nawe; wala sili chakula wala sinywi maji pamoja nawe hapa;
17 kwani nimeambiwa kwa neno la Bwana, Usile chakula wala usinywe maji huko, wala usirudi kwa njia ile uliyoijia.
18 Akamwambia, Mimi nami ni nabii kama wewe, na malaika akaniambia kwa neno la Bwana, kusema, Mrudishe pamoja nawe nyumbani kwako, ale chakula, akanywe maji. Lakini alisema uongo.
19 Basi mtu yule akarudi pamoja naye, akala chakula, akanywa maji nyumbani mwake.
20 Hata ikawa, walipokuwa wameketi mezani, neno la Bwana likamjia nabii yule aliyemrudisha;
21 akamlilia yule mtu wa Mungu aliyetoka katika Yuda, akinena, Bwana asema hivi, Kwa sababu umeiasi kauli ya Bwana, wala hukuishika amri ile aliyokuamuru Bwana, Mungu wako,
22 bali umerudi, ukala chakula ukanywa maji, hapo alipokuambia, Usile chakula, wala usinywe maji; maiti yako haitaliingia kaburi la baba zako.
23 Basi ikawa, alipokwisha kula chakula na kunywa maji, yule nabii aliyemrudisha akamtandikia punda.
24 Na alipokuwa amekwenda zake, simba alimkuta njiani, akamwua. Maiti yake ikatupwa njiani, na yule punda akasimama karibu naye; na yule simba naye akasimama karibu na maiti.
25 Na tazama, watu wakapita, wakauona mzoga umetupwa njiani, na yule simba akisimama karibu na mzoga, wakaenda, wakatoa habari katika mji ule alimokaa yule nabii mzee.
26 Na yule nabii aliyemrudisha njiani alipopata habari, akasema; Ndiye yule mtu wa Mungu, aliyeiasi kauli ya Bwana; kwa hiyo Bwana amempambanisha na simba, simba akamrarua, akamwua, sawasawa na neno la Bwana alilomwambia.
27 Akawaambia wanawe, akasema, Nitandikieni punda. Wakamtandikia.
28 Akaenda, akamwona yule maiti ametupwa njiani, na punda na simba wamesimama karibu na maiti; yule simba alikuwa hakumla maiti, wala hakumrarua punda.
29 Nabii yule akamtwaa maiti wa yule mtu wa Mungu, akamweka juu ya punda wake, akamrudisha; yule nabii mzee akaenda mjini mwake, kukaa matanga, na kumzika.
30 Akamweka maiti katika kaburi lake mwenyewe; wakamlilia, wakisema, Aa! Ndugu yangu!
31 Hata ikawa, alipokwisha kumzika, akawaambia wanawe, akasema, Nikifa mimi, nizikeni katika kaburi hili alimozikwa yule mtu wa Mungu; iwekeni mifupa yangu kando ya mifupa yake.
32 Kwa maana neno hilo alilolia juu ya madhabahu katika Betheli, kwa neno la Bwana, na juu ya nyumba zote za mahali pa juu zilizo katika miji ya Samaria, hakika litatimizwa.
33 Baada ya hayo Yeroboamu hakuiacha njia yake mbovu, lakini akafanya tena makuhani wa mahali pa juu, wa watu wo wote.
34 Kila aliyetaka akamfanya wakfu, ili wawepo makuhani wa mahali pa juu. Jambo hilo likawa dhambi kwa nyumba ya Yeroboamu, hata kuiharibu, na kuifuta usoni pa nchi.