1 Wakorintho 4
1 Mtu na atuhesabu hivi, kuwa tu watumishi wa Kristo, na mawakili wa siri za Mungu.
2 Hapo tena inayohitajiwa katika mawakili, ndiyo mtu aonekane kuwa mwaminifu.
3 Lakini, kwangu mimi, si kitu kabisa nihukumiwe na ninyi, wala kwa hukumu ya kibinadamu, wala sijihukumu hata nafsi yangu.
4 Maana sijui sababu ya kujishitaki nafsi yangu, lakini sihesabiwi haki kwa ajili hiyo; ila anihukumuye mimi ni Bwana.
5 Basi ninyi msihukumu neno kabla ya wakati wake, hata ajapo Bwana; ambaye atayamulikisha yaliyositirika ya giza, na kuyadhihirisha mashauri ya mioyo; ndipo kila mtu atakapoipata sifa yake kwa Mungu.
6 Basi ndugu, mambo hayo nimeyafanya kuwa mfano wa mimi na Apolo kwa ajili yenu, ili kwamba kwa mfano wetu mpate kujifunza kutokupita yale yaliyoandikwa; ili mmoja wenu asijivune kwa ajili ya huyu, kinyume cha mwenziwe.
7 Maana ni nani anayekupambanua na mwingine? Nawe una nini usichokipokea? Lakini iwapo ulipokea, wajisifia nini kana kwamba hukupokea?
8 Mmekwisha kushiba, mmekwisha kupata utajiri, mmemiliki pasipo sisi. Naam, laiti mngemiliki, ili sisi nasi tumiliki pamoja nanyi!
9 Maana nadhani ya kuwa Mungu ametutoa sisi mitume mwisho, kama watu waliohukumiwa wauawe; kwa sababu tumekuwa tamasha kwa dunia; kwa malaika na wanadamu.
10 Sisi tu wapumbavu kwa ajili ya Kristo, lakini ninyi ni wenye akili katika Kristo; sisi tu dhaifu, lakini ninyi mna nguvu; ninyi mna utukufu, lakini sisi hatupati heshima.
11 Hata saa hii ya sasa, tuna njaa na kiu, tu uchi, twapigwa ngumi, tena hatuna makao;
12 kisha twataabika tukifanya kazi kwa mikono yetu wenyewe. Tukitukanwa twabariki, tukiudhiwa twastahimili;
13 tukisingiziwa twasihi; tumefanywa kama takataka za dunia, na tama ya vitu vyote hata sasa.
14 Siyaandiki hayo ili kuwatahayarisha; bali kuwaonya kama watoto niwapendao.
15 Kwa kuwa ijapokuwa mna waalimu kumi elfu katika Kristo, walakini hamna baba wengi. Maana mimi ndimi niliyewazaa katika Kristo Yesu kwa njia ya Injili.
16 Basi, nawasihi mnifuate mimi.
17 Kwa sababu hii nimemtuma Timotheo kwenu, aliye mwanangu mpendwa, mwaminifu katika Bwana, atakayewakumbusha njia zangu zilizo katika Kristo, kama vile nifundishavyo kila mahali katika kila kanisa.
18 Basi wengine wamejivuna kana kwamba siji kwenu.
19 Lakini nitakuja kwenu upesi, nikijaliwa, nami nitafahamu, si neno lao tu waliojivuna, bali nguvu zao.
20 Maana ufalme wa Mungu hauwi katika neno, bali katika nguvu.
21 Mnataka vipi? Nije kwenu na fimbo, au nije katika upendo na roho ya upole?