1 Wakorintho 16
1 Kwa habari ya ile changizo kwa ajili ya watakatifu, kama vile nilivyoamuru makanisa ya Galatia, nanyi fanyeni vivyo.
2 Siku ya kwanza ya juma kila mtu kwenu na aweke akiba kwake, kwa kadiri ya kufanikiwa kwake; ili kwamba michango isifanyike hapo nitakapokuja;
3 nami nitakapofika nitawatuma kwa nyaraka wale mtakaowachagua, wachukue hisani yenu mpaka Yerusalemu.
4 Na kama ikifaa niende na mimi, watasafiri pamoja nami.
5 Lakini nitakuja kwenu, nikiisha kupita kati ya Makedonia; maana napita kati ya Makedonia.
6 Labda nitakaa kwenu; naam, labda wakati wote wa baridi, mpate kunisafirisha ko kote nitakakokwenda.
7 Maana sipendi kuonana nanyi sasa, katika kupita tu, kwa sababu nataraji kukaa kwenu muda kidogo, Bwana akinijalia.
8 Lakini nitakaa Efeso hata Pentekoste;
9 kwa maana nimefunguliwa mlango mkubwa wa kufaa sana, na wako wengi wanipingao.
10 Lakini, Timotheo akija, angalieni akae kwenu pasipo hofu; maana anaifanya kazi ya Bwana vile vile kama mimi mwenyewe;
11 basi mtu ye yote asimdharau, lakini msafirisheni kwa amani, ili aje kwangu; maana ninamtazamia pamoja na ndugu zetu.
12 Lakini kwa habari za Apolo, ndugu yetu, nalimsihi sana aende kwenu pamoja na hao ndugu; ambaye si mapenzi yake kwenda sasa; lakini atakuja atakapopata nafasi.
13 Kesheni, simameni imara katika Imani, fanyeni kiume, mkawe hodari.
14 Mambo yenu yote na yatendeke katika upendo.
15 Tena ndugu, nawasihi; (mnawajua watu wa nyumbani mwa Stefana kwamba ni malimbuko ya Akaya, nao wamejitia katika kazi ya kuwahudumu watakatifu);
16 watiini watu kama hawa, na kila mtu afanyaye kazi pamoja nao, na kujitaabisha.
17 Nami nafurahi kwa sababu ya kuja kwao Stefana na Fortunato na Akaiko; maana hawa wamenikirimia kwa wingi yale niliyopungukiwa kwenu.
18 Maana wameniburudisha roho yangu, na roho zenu pia; basi wajueni sana watu kama hao.
19 Makanisa ya Asia wawasalimu. Akila na Priska wawasalimu sana katika Bwana, pamoja na kanisa lililoko ndani ya nyumba yao.
20 Ndugu wote wawasalimu. Salimianeni kwa busu takatifu.
21 Hii ni salamu yangu Paulo kwa mkono wangu mwenyewe.
22 Mtu awaye yote asiyempenda Bwana, na awe amelaaniwa. Maran atha.
23 Neema ya Bwana Yesu na iwe pamoja nanyi.
24 Pendo langu na liwe pamoja nanyi nyote katika Kristo Yesu.