1 Wakorintho 14
1 Ufuateni upendo, na kutaka sana karama za rohoni, lakini zaidi kwamba mpate kuhutubu.
2 Maana yeye anenaye kwa lugha, hasemi na watu, bali husema na Mungu; maana hakuna asikiaye; lakini anena mambo ya siri katika roho yake.
3 Bali yeye ahutubuye, asema na watu maneno ya kuwajenga, na kuwafariji, na kuwatia moyo.
4 Yeye anenaye kwa lugha hujijenga nafsi yake; bali ahutubuye hulijenga kanisa.
5 Nami nataka ninyi nyote mnene kwa lugha, lakini zaidi sana mpate kuhutubu, maana yeye ahutubuye ni mkuu kuliko yeye anenaye kwa lugha, isipokuwa afasiri, ili kusudi kanisa lipate kujengwa.
6 Ila sasa, ndugu, nikija kwenu na kunena kwa lugha, nitawafaidia nini, isipokuwa nasema nanyi kwa njia ya ufunuo, au kwa njia ya elimu, au kwa njia ya hotuba, au kwa njia ya fundisho?
7 Hata vitu visivyo na uhai vitoapo sauti, ikiwa ni filimbi, ikiwa ni kinubi, visipotoa sauti zilizo na tofauti, itatambulikanaje ni wimbo gani unaopigwa kwa filimbi au kwa kinubi?
8 Kwa maana baragumu ikitoa sauti isiyojulikana, ni nani atakayejifanya tayari kwa vita?
9 Vivyo hivyo na ninyi, msipotoa kwa ulimi neno lililo dhahiri, neno lile linenwalo litajulikanaje? Maana mtakuwa mkinena hewani tu.
10 Yamkini ziko sauti za namna nyingi duniani, wala hakuna moja isiyo na maana.
11 Basi nisipoijua maana ya ile sauti nitakuwa kama mjinga kwake yeye anenaye; naye anenaye atakuwa mjinga kwangu.
12 Vivyo hivyo na ninyi, kwa kuwa mnatamani sana kuwa watu wenye karama za roho, takeni kwamba mzidi sana kuwa nazo ili kulijenga kanisa.
13 Kwa sababu hiyo yeye anenaye kwa lugha na aombe apewe kufasiri.
14 Maana nikiomba kwa lugha, roho yangu huomba, lakini akili zangu hazina matunda.
15 Imekuwaje, basi? Nitaomba kwa roho, tena nitaomba kwa akili pia; mtaimba kwa roho, tena nitaimba kwa akili pia.
16 Kwa maana wewe ukibariki kwa roho, yeye aketiye katika mahali pa mjinga ataitikaje, Amina, baada ya kushukuru kwako, akiwa hayajui usemayo?
17 Maana ni kweli, wewe washukuru vema, bali yule mwingine hajengwi.
18 Namshukuru Mungu ya kuwa nanena kwa lugha zaidi ya ninyi nyote;
19 lakini katika kanisa napenda kunena maneno matano kwa akili zangu, nipate kuwafundisha wengine, zaidi ya kunena maneno kumi elfu kwa lugha.
20 Ndugu zangu, msiwe watoto katika akili zenu; lakini katika uovu mgeuzwe watoto wachanga, bali katika akili zenu mkawe watu wazima.
21 Imeandikwa katika torati, Nitasema na watu hawa kwa watu wa lugha nyingine, na kwa midomo ya wageni, wala hata hivyo hawatanisikia, asema Bwana.
22 Basi, hizi lugha ni ishara, si kwao waaminio, bali kwao wasioamini lakini kuhutubu si kwa ajili yao wasioamini, bali kwa ajili yao waaminio.
23 Haya! Ikiwa kanisa lote limekusanyika pamoja, na wote wanene kwa lugha, kisha ikawa wameingia watu wajinga au wasioamini, je! Hawatasema ya kwamba mna wazimu?
24 Lakini wote wakihutubu, kisha akaingia mtu asiyeamini, au mjinga, abainishwa na wote, ahukumiwa na wote;
25 siri za moyo wake huwa wazi; na hivyo atamwabudu Mungu, akianguka kifudifudi, na kukiri ya kuwa Mungu yu kati yenu bila shaka.
26 Basi, ndugu, imekuwaje? Mkutanapo pamoja, kila mmoja ana zaburi, ana fundisho, ana ufunuo, ana lugha, ana tafsiri. Mambo yote na yatendeke kwa kusudi la kujenga.
27 Kama mtu akinena kwa lugha, wanene wawili au watatu, si zaidi, tena zamu kwa zamu, na mmoja na afasiri.
28 Lakini asipokuwapo mwenye kufasiri na anyamaze katika kanisa; aseme na nafsi yake tena na Mungu.
29 Na manabii wanene wawili, au watatu, na wengine wapambanue.
30 Lakini mwingine aliyeketi akifunuliwa neno, yule wa kwanza na anyamaze.
31 Kwa maana ninyi nyote mwaweza kuhutubu mmoja mmoja, ili wote wapate kujifunza, na wote wafarijiwe.
32 Na roho za manabii huwatii manabii.
33 Kwa maana Mungu si Mungu wa machafuko, bali wa amani; vile vile kama ilivyo katika makanisa yote ya watakatifu.
34 Wanawake na wanyamaze katika kanisa, maana hawana ruhusa kunena bali watii, kama vile inenavyo torati nayo.
35 Nao wakitaka kujifunza neno lo lote, na wawaulize waume zao wenyewe nyumbani mwao; maana ni aibu wanawake kunena katika kanisa.
36 Au je! Neno la Mungu lilitoka kwenu? Au kuwafikia ninyi peke yenu?
37 Mtu akijiona kuwa ni nabii au mtu wa rohoni, na ayatambue hayo ninayowaandikia, ya kwamba ni maagizo ya Bwana.
38 Lakini mtu akiwa mjinga, na awe mjinga.
39 Kwa ajili ya hayo, ndugu, takeni sana kuhutubu, wala msizuie kunena kwa lugha.
40 Lakini mambo yote na yatendeke kwa uzuri na kwa utaratibu.