«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »

1 Wakorintho 13

1  Nijaposema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo, nimekuwa shaba iliayo na upatu uvumao.

2  Tena nijapokuwa na unabii, na kujua siri zote na maarifa yote, nijapokuwa na imani timilifu kiasi cha kuweza kuhamisha milima, kama sina upendo, si kitu mimi.

3  Tena nikitoa mali zangu zote kuwalisha maskini, tena nikijitoa mwili wangu niungue moto, kama sina upendo, hainifaidii kitu.

4  Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari; haujivuni;

5  haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya;

6  haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli;

7  huvumilia yote; huamini yote; hutumaini yote; hustahimili yote.

8  Upendo haupungui neno wakati wo wote; bali ukiwapo unabii utabatilika; zikiwapo lugha, zitakoma; yakiwapo maarifa, yatabatilika.

9  Kwa maana tunafahamu kwa sehemu; na tunafanya unabii kwa sehemu;

10  lakini ijapo ile iliyo kamili, iliyo kwa sehemu itabatilika.

11  Nilipokuwa mtoto mchanga, nalisema kama mtoto mchanga, nalifahamu kama mtoto mchanga, nalifikiri kama mtoto mchanga; tokea hapo nilipokuwa mtu mzima, nimeyabatilisha mambo ya kitoto.

12  Maana wakati wa sasa tunaona kwa kioo kwa jinsi ya fumbo; wakati ule tutaona uso kwa uso; wakati wa sasa nafahamu kwa sehemu; wakati ule nitajua sana kama mimi nami ninavyojuliwa sana.

13  Basi, sasa inadumu imani, tumaini, upendo, haya matatu; na katika hayo lililo kuu ni upendo.

«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »
“Neema ya Bwana Yesu na iwe pamoja nanyi.” — 1 Wakorintho 16:23