1 Mambo ya Nyakati 28
1 Kisha Daudi akawakusanya huko Yerusalemu wakuu wote wa Israeli, wakuu wa kabila, na maakida wa vikosi wenye kumtumikia mfalme kwa zamu, na maakida wa maelfu, na maakida wa mamia, na wenye kutawala juu ya mali na milki za mfalme, na za wanawe, pamoja na matowashi, na mashujaa, naam, waume mashujaa wote.
2 Ndipo Daudi mfalme akasimama kwa miguu yake, akasema, Nisikilizeni, ndugu zangu, na watu wangu; Mimi nalikuwa na nia ya kuijenga nyumba ya kustarehe kwa ajili ya sanduku la agano la Bwana, na kiti cha kuwekea miguu yake cha Mungu wetu; hata nalikuwa nimeweka tayari kwa kujenga.
3 Lakini Mungu akaniambia, Wewe hutajenga nyumba kwa ajili ya jina langu, kwa sababu umekuwa mtu wa vita, nawe umemwaga damu.
4 Walakini Bwana, Mungu wa Israeli, alinichagua katika nyumba yote ya babangu kuwa mfalme juu ya Israeli milele, kwa kuwa amemchagua Yuda awe mkuu; na katika nyumba ya Yuda, alichagua nyumba ya babangu, na miongoni mwa wana wa babangu, aliniridhia mimi ili kunitawaza niwe mfalme juu ya Israeli wote;
5 tena katika wana wangu wote (kwani Bwana amenipa wana wengi), amemchagua Sulemani mwanangu ili aketi juu ya kiti cha enzi cha ufalme wa Bwana, juu ya Israeli.
6 Akaniambia, Sulemani, mwanao, ndiye atakayeijenga nyumba yangu na nyua zangu; kwa kuwa nimemchagua awe mwanangu, nami nitakuwa babaye.
7 Na ufalme wake nitauweka imara milele, akijitia kwa bidii kuzitenda amri zangu na hukumu zangu, kama hivi leo.
8 Basi sasa, machoni pa Israeli wote, hilo kusanyiko la Bwana, na masikioni pa Mungu wetu, angalieni na kuzitafuta amri zote za Bwana, Mungu wenu, ili mpate kuimiliki nchi hii njema, na kuwarithisha wana wenu baada yenu hata milele.
9 Nawe, Sulemani mwanangu, mjue Mungu wa baba yako, ukamtumikie kwa moyo mkamilifu, na kwa nia ya kumkubali; kwa kuwa Bwana hutafuta-tafuta mioyo yote, na kuyatambua mawazo yote ya fikira; ukimtafuta, ataonekana nawe; ukimwacha, atakutupa milele.
10 Jihadhari basi; kwani Bwana amekuchagua wewe ili ujenge nyumba itakayokuwa mahali patakatifu; uwe hodari ukatende hivyo.
11 Ndipo Daudi akampa Sulemani mwanawe mfano wa ukumbi wa hekalu, na nyumba zake, na hazina zake, na orofa zake, na vyumba vyake vya ndani, na mahali pa kiti cha rehema;
12 na mfano wa yote aliyokuwa nayo kwa roho, katika habari ya nyua za nyumba ya Bwana, na ya vyumba vyote vilivyoizunguka, ya hazina za nyumba ya Mungu, na ya hazina za vitu vilivyowekwa wakfu;
13 tena katika habari ya zamu za makuhani na Walawi, na ya kazi yote ya huo utumishi wa nyumba ya Bwana, na ya vyombo vyote vya utumishi nyumbani mwa Bwana;
14 ya dhahabu kwa uzani kwa vyombo vya dhahabu, kwa vyombo vyote vya utumishi wa kila namna; ya fedha kwa uzani kwa vyombo vyote vya fedha, kwa vyombo vyote vya utumishi wa kila namna;
15 kwa uzani tena kwa vinara vya dhahabu, na kwa taa zake za dhahabu, kwa uzani, kwa kila kinara, na kwa taa zake; na kwa vinara vya fedha, kwa uzani kwa kila kinara na kwa taa zake, kwa kadiri ya matumizi ya kila kinara;
16 na dhahabu kwa uzani kwa meza za mikate ya wonyesho, kwa kila meza; na fedha kwa meza za fedha;
17 na nyuma, na mabakuli, na vikombe vya dhahabu safi; na kwa matasa ya dhahabu, kwa uzani kwa kila tasa; na kwa matasa ya fedha, kwa uzani kwa kila tasa;
18 na kwa madhabahu ya kufukizia, dhahabu iliyosafika sana kwa uzani; na dhahabu kwa mfano wa gari, yaani, makerubi, yenye kutandaza mabawa, na kulifunika sanduku la agano la Bwana.
19 Hayo yote, akasema Daudi, yamenielea kwa maandiko kutoka kwa mkono wa Bwana, naam, kazi zote za mfano huu.
20 Kisha Daudi akamwambia Sulemani mwanawe, Uwe hodari, mwenye moyo mkuu, ukatende hivyo; usiogope wala usifadhaike; kwa kuwa Bwana, Mungu, Mungu wangu, yu pamoja nawe; yeye hatakupungukia wala kukuacha, hata itakapomalizika kazi yote ya huo utumishi wa nyumba ya Bwana.
21 Na tazama, hizo zamu za makuhani na Walawi ziko, kwa utumishi wote wa nyumba ya Mungu; nao watakuwapo pamoja nawe kwa kazi ya kila namna, kila mtu mwenye hiari, aliye stadi kwa utumishi wo wote; tena maakida na watu wote watakuwa chini ya amri yako kabisa.