«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »

1 Mambo ya Nyakati 14

1  Naye Hiramu, mfalme wa Tiro, akatuma wajumbe kwa Daudi, akampelekea na mierezi, na waashi, na maseremala, ili wamjengee nyumba.

2  Daudi akajua ya kwamba Bwana amemweka imara ili amiliki juu ya Israeli, kwa kuwa milki yake imeinuka kwa ajili ya watu wake Israeli.

3  Tena Daudi akazidi kuoa wake huko Yerusalemu; akazidi Daudi kuzaa wana na binti.

4  Na haya ndiyo majina ya watoto aliozaliwa huko Yerusalemu; Shamua, na Shobabu, na Nathani, na Sulemani;

5  na Ibhari, na Elishua, na Elpeleti;

6  na Noga, na Nefegi, na Yafia;

7  na Elishama, na Eliada, na Elifeleti.

8  Na waliposikia hao Wafilisti ya kwamba Daudi ametiwa mafuta ili awe mfalme juu ya Israeli wote, Wafilisti wote wakapanda kumtafuta Daudi; naye Daudi akasikia, akatoka nje kupigana nao.

9  Basi hao Wafilisti walikuwa wamekuja na kuteka nyara katika bonde la Warefai.

10  Daudi akamwuliza Mungu, kusema, Je! Nipande juu ya Wafilisti! Utawatia mikononi mwangu? Naye Bwana akamwambia, Panda; kwa kuwa nitawatia mikononi mwako.

11  Basi wakapanda mpaka Baal-perasimu, Daudi naye akawapiga huko; Daudi akasema, Bwana amewafurikia adui zangu kwa mkono wangu, kama mafuriko ya maji. Basi wakapaita mahali pale jina lake Baal-perasimu.

12  Nao wakaiacha miungu yao huko; naye Daudi akaamuru, ikateketezwa kwa moto.

13  Lakini hao Wafilisti wakateka nyara tena mara ya pili bondeni.

14  Na Daudi akamwuliza Mungu tena; naye Mungu akamwambia, Hutapanda kuwafuata; uwageukie mbali, ukawajie huko kuielekea miforsadi.

15  Kisha itakuwa utakapoisikia sauti ya kwenda katika vilele vya miforsadi, ndipo utakapokwenda nje vitani; kwa maana ndipo Mungu ametoka mbele yako, awapige jeshi la Wafilisti.

16  Daudi akafanya kama vile Mungu alivyomwamuru; wakawapiga jeshi la Wafilisti toka Geba mpaka Gezeri.

17  Sifa za Daudi zikafika nchi zote; naye Bwana akawaletea mataifa yote hofu yake.

«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »
“Neema ya Bwana Yesu na iwe pamoja nanyi.” — 1 Wakorintho 16:23